Full-Width Version (true/false)


Makusanyo ya Serikali kupanda sababu hiiMamlaka ya Mapato (TRA) imetaja sababu nne zilizosababisha makusanyo ya kodi kuongezeka kutoka Sh. trilioni 14.4 mwaka wa fedha 2016/17 hadi kufikia Sh. trilioni 15.5 mwaka 2017/18.


Lengo la serikali kwa mwaka huo wa fedha lilikuwa mamlaka hiyo ikusanye Sh. trilioni 17.1.Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu makusanyo ya kodi kwa mwaka 2017/18, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na elimu ya kodi kuzidi kueleweka kwa walipakodi na wananchi.


Alisema sababu nyingine ni TRA kuongeza ukaribu na walipakodi kwa kuwasikiliza na kutatua changamoto zao za kikodi, kuongezeka kwa walipakodi wapya kupitia kampeni ya kuwasajili kwa kuwafuata waliko na kurahisisha ulipaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki.


“TRA imefanikiwa kukusanya Sh. trilioni 15.5 kwa mwaka mzima wa fedha wa 2017/18 kuanzia Julai 2017 hadi Juni 2018 ikilinganishwa na Sh. trilioni 14.4 ambazo zilikusanywa katika mwaka wa fedha 2016/17. Kiasi hiki ni sawa na ukuaji wa asilimia 7.5,” alisema Kayombo.


Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mwezi uliopita uliokuwa wa mwisho kwa mwaka wa fedha 2017/18, TRA ilikusanya Sh. trilioni 1.5 ikilinganishwa na Sh. trilioni 1.4 kwa mwezi Juni 2017, sawa na ukuaji wa asilimia nane.


Alisema malengo ya TRA kwa mwaka wa fedha 2018/19 ni kutekeleza kwa vitendo kampeni ya msamaha wa riba na adhabu kwa malimbikizo ya madeni ya nyuma, ili kuongeza urahisi wa kulipa madeni ambayo yalikuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wengi kulipa na hata kuendelea na biashara.


“Kuanzia sasa hadi Novemba 30, mwaka huu, ndiyo mwisho wa siku ya kuomba msamaha wa kufutiwa madeni na malimbikizo ya kodi na Juni 30, 2019 ndiyo mwisho wa kulipa madeni ya kodi,” alisema Kayombo.


Aliongeza kuwa wamedhamiria kuongeza kasi ya usajili wa walipakodi wapya pamoja na kuendelea na kasi ya utambuzi na usajili wa wafanyabiashara wadogo, ili wasajiliwe katika mfumo wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.


Kayombo alisema fedha zinazokusanywa na TRA zinatumika katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na za kijamii zikiwamo ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara, ununuzi wa ndege, upatikanaji wa elimu, afya na mambo mengine kwa manufaa ya Watanzania.


Katika mchanganuo wake kuhusu makusanyo ya kodi kwa miezi yote 12 ya mwaka wa fedha 2017/18, Kayombo alibainisha kuwa Januari 2018, TRA ilikusanya Sh. trilioni 1.23, Februari Sh. trilioni 1.167, Machi Sh. trilioni 1.534, Aprili Sh. trilioni 1.078, Mei Sh. trilioni 1.132, Juni Sh. trilioni 1.516.


Alisema Julai 2017, TRA ilikusanywa Sh. trilioni 1.01, Agosti Sh. trilioni 1.205, Septemba Sh. trilioni 1.345, Oktoba Sh. trilioni 1.293 , Novemba Sh. trilioni 1.264, na Desemba Sh. trilioni 1.63.

No comments

Powered by Blogger.