Full-Width Version (true/false)


Manispaa yamsaka aliyemzuia mjasiriamali kuuza uji Sabasaba
Manispaa ya Temeke imesema inafanyia kazi malalamiko ya mjasiriamali, Stumai Simba anayedai kuzuiwa kuuza uji katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) ya Sabasaba.
Mjasiriamali huyo amezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya taarifa zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa mtu aliyejitambulisha kuwa ofisa afya wa Manispaa ya Temeke alimzuia kuuza uji kwa kutokuwa na cheti cha ofisi yake.
Stumai alisema jana kuwa alimweleza ofisa afya huyo kuwa alikuwa na kibali cha Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) lakini hakukubaliana naye na badala yake alituma askari polisi ambao walimtoa uwanjani.
Akizungumzia suala hilo jana, Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke, Hashim Komba alisema anazo taarifa za tukio hilo na kwamba anazifuatilia kwa karibu na ukweli ukibainika, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mhusika.
“Taarifa tumezipata japo kwa kuchelewa, tunazifanyia kazi kwa karibu. Mimi nilipata nafasi ya kukutana na binti huyo jana (juzi) akanielezea changamoto hiyo,” alisema Komba.
Alisema bado wanamtafuta ofisa afya huyo na taarifa za awali zinaonyesha kuwa ni wa Kata ya Keko kwa kuwa ndiye aliyekuwa amepangiwa kufanya kazi Sabasaba.
Komba alisema atakutana na ofisa afya wa Manispaa ya Temeke ili kusikiliza upande wa pili kabla ya kuchukua hatua.
“Si dhamira ya Serikali kuwanyanyasa wajasiriamali wadogo. Wajibu wa Serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi,” alisema.
Mjasiriamali huyo alisema ofisa huyo alikwenda eneo alilokuwa akifanyia biashara na kumtaka awe na cheti cha manispaa vinginevyo aondoke.
Alisema alipeleka malalamiko TFDA ambao walikuwapo kwenye maonyesho hayo ambao alisema walieleza kushangazwa kwao na hatua hiyo kwa kuwa walishampa kibali baada ya kujiridhisha kwamba mazingira yake ya biashara ni safi.
Mjasiriamali huyo alisema Julai 8 alilazimika kumwaga zaidi ya vikombe 300 vya uji na aliendelea kuwalipa wasaidizi wake licha ya kwamba hakufanya biashara.
Mwanaharakati wa haki za wanawake na mwanzilishi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu suala hilo akisema mtu anapoamua kujiajiri, mamlaka zinapaswa kuweka mazingira rafiki ya kufanya shughuli zake.

No comments

Powered by Blogger.