Full-Width Version (true/false)


Mbadala wa soko la mbaazi wapatikanaWAKATI wakulima wa zao la mbaazi nchini wakilalamikia  kukosekana kwa soko la nje, wakulima wa zao hilo wilayani Kilosa mkoani Morogoro, wamebuni mbinu mpya kwa  kutengeneza bidhaa zinazotokana na zao hilo. 

Miongoni mwa bidhaa hizo zinazotengenezwa kupitia zao hilo ni bagia, unga wa lishe unaochanganywa na virutubisho, kahawa ya mbaazi na kutengeneza supu kama chakula kwa kutumia mbaazi na kuuzwa katika mahoteli. 

Wakizungumza katika maonyesho ya teknolojia za kilimo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Ilonga wilayani Kilosa, wakulima wa mbaazi walisema walianza kutengeneza bidhaa hizo tangu mwaka jana. 

Juma Ramadhani kutoka Kijiji cha Peapea, alisema ubunifu wa kutengeneza vyakula vinavyotokana na mbaazi umetokana na kuporomoka kwa soko hilo, ambapo awali walikuwa wakiuza kwa kampuni za nje kwa gunia moja Sh. 300,000 mpaka 400,000. 

Alisema msimu wa kilimo wa mwaka 2014/15 na 16 kwa wakulima wa mbaazi Kilosa ulikuwa na manufaa makubwa kwao, kwani waliweza kujiingizia kipato kwa wingi tofauti na msimu wa mwaka 2017, ambao ulikuwa kilio kwao kutokana na zao hilo kukosa soko la uhakika. Mariam Juma kutoka Kijiji cha Rudewa, alisema hawatakata tamaa na kuacha kulima zao hilo, kwa kuwa wameshabuni soko ambalo limeanza kueleweka wakati wakisubiri utaratibu wa serikali wa kuwatafutia masoko nje ya nchi. 

Mtafiti mkuu wa mazao ya mbaazi na mikunde kutoka TARI Ilonga, Meshack Makenge, alisema wakulima wamefundishwa utaalamu wa kuangalia soko la ndani, ili kupitia zao la mbaazi wanaweza kutumia kutengeneza vyakula mbalimbali, ambavyo vingine vitatumika kama sehemu ya biashara na kuwaingizia kipato wakati serikali ikiendelea kuweka mipango rafiki ya soko. 

Alisema wakulima wa Wilaya za Kilosa na Gairo hawana tatizo la soko kwa kuwa wamekuwa wakitengeneza vyakula vinavyotokana na mbaazi na kuviuza katika maduka makubwa na mahoteli. Mkurugenzi wa bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko, Dk. Hussein Mansoour, alisema licha ya serikali kuendelea kutafuta masoko nje, lakini tumeweka utaratibu wa kuanza ujenzi wa viwanda vya mazao ya mikunde ikiwamo mbaazi katika Mkoa wa Morogoro na kuwa mwekezaji ameshapatikana.

No comments

Powered by Blogger.