Full-Width Version (true/false)


Mbelgiji Simba awatega Kagere, Okwi
SAA chache kabla ya kutua nchini kuanza kazi Msimbazi, Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems, amewatumia ujumbe mabosi wa klabu hiyo akitaka wawafikishie salamu nyota wa kikosi hicho akiwamo Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi.
Kocha huyo anayetarajiwa kutua nchini usiku wa kesho Jumanne kabla ya kufichwa katika hoteli moja matata akisubiri mipango ya safari na vijana wake kwenda kambini nchini Uturuki, amewataka viongozi kuhakikisha nyota wote wanakuwepo huku akisisitiza kuwa kwake hakuna supastaa wala nini, anataka watu wa kazi.
Mbelgiji huyo amemwambia mmoja wa vigogo waliohusika kumleta nchini kuwa kabla ya kuondoka kwenda katika maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara huko Uturuki, anataka kuonana na wachezaji wote wa kikosi hicho azungumze nao.
Kigogo huyo alidokeza kuwa kocha Aussems anataka kuongea na nyota wake hao ili awaambie wasahau ya msimu uliopita na kuanza kujipanga upya kwa msimu ujao chini ya mikono yake.
“Jamaa anaonesha yupo makini na kazi yake kwani aliniambia anataka kuonana na wachezaji kabla hatujaenda Uturuki ili aongee nao wajue kuwa kazi ndio inaanza, “ alisema kigogo huo.
“Amesisitiza akiwa kambini ataangalia mchezaji anayejituma, nidhamu, hivyo nyota wa Simba waanze kujipanga mapema sasa.”
Kauli hiyo inamaanisha huenda wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza chini ya kocha Pierre Lechantre wakikomaa watapata namba na mafaza watakaokuwa wanaringia jina inaweza kula kwao kwa Mbelgiji huyo.
Ukiondoa Meddie Kagere aliyetua hivi karibuni na kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba, Wekundu inao nyota wengine wenye majina makubwa waliotamba msimu uliiopita akiwamo Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya.
MSIKIE RAIS
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kama mabosi wa Simba wamejipanga kuhakikisha benchi la ufundi linatekelezewa kila wanachokitaka na hawataingilia majukumu ya makocha Aussems na wasaidizi wake.
Naye Meneja wa timu hiyo, Richard Robert, amesema mipango ya safari ipo hatua nzuri na huenda msafara wao ukahusisha wachezaji 25 ila wanaweza kuongeza ili waende wote kama utaratibu utakwenda sawa.
Simba imepanga kuondoka Ijumaa ili kwenda huko kujiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika.
GARI LA SALAMBA NYANG’ANYANG’A
Wakati huohuo gari la kisasa la straika mpya wa Simba, Adam Salamba, limeharibika vibaya baada ya kugongwa eneo la Vigwaza, mkoani Pwani likiwa linaendeshwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Nassoro Masoud ‘Cholo’.
Cholo aliyekuwa peke yake garini, alipata ajali hiyo wakati akitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam baada ya kugongwa kwa nyuma kabla ya kuvamia gari jingine mbele.
Cholo alisema Salamba alimuomba akamchukulie gari hilo ili amletee Dar.

No comments

Powered by Blogger.