Full-Width Version (true/false)


Mfumuko wa bei wapungua

 


OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetoa hali ya mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Juni, mwaka huu, ambao umeonyesha kupungua hadi kufikia asilimia 3.4 ikilinganishwa na mwezi Mei iliyokuwa asilimia 3.6. Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa NBS, Ephraim Kwesigabo, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Juni, mwaka huu. 

"Mfumuko wa bei wa taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini, mfumuko wa bei kwa mwezi Juni umepungua hadi kufikia asilimia 3.4 ikilinganishwa na asilimia 3.6 ilivyokuwa mwezi Mei," alisema Kwesigabo. 

Alisema hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018 imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018. 

Kwesigabo alitaja sababu zilizosababisha kupungua kwa mfumuko wa bei ni kupungua kwa mfumuko wa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula ambazo ni bia kwa asilimia 1.1, gharama za ukarabati wa vifaa vya umeme na viyoyozi kwa asilimia 1.8. 

Bidhaa zingine ni gesi za kupikia majumbani kwa asilimia 5.6, majiko ya mkaa kwa asilimia 2.0, na gharama za mawasiliano kwa asilimia 2.6. Kuhusu mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, Kwesigabo alisema kwa nchi ya Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018 umeongezeka kidogo hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018. 

Alisema failisi za bei nazo zimepungua hadi -2.4 kulikosababishwa na kupungua kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula ambazo ni bia, gesi, mawasiliano, majiko ya mkaa pamoja na vifaa vya umeme. 

Alisema kwa nchi ya Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018 umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.28 kutoka asilimia 3.95 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018.

No comments

Powered by Blogger.