Full-Width Version (true/false)


Mkongo apewa mikoba ya Ngoma
JEZI namba 11 ya Yanga ambayo ilikuwa ikitumiwa na straika mpya wa Azam FC, Donald Ngoma, sasa itavaliwa na straika wao mpya Mkongomani, Heritier Makambo.
Usajili wa Makambo aliyetokea FC Lupopo unakuwa wa tatu kwa Yanga, baada ya kumnasa kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohamed Issah Banka na Feisal Salum.
Imeelezwa kuwa Makambo anachukuwa nafasi ya Ngoma na kupewa jezi hiyo ambayo ilikuwa haina mtu klabuni hapo baada ya Ngoma kuanza kuzingua kisha kutimkia zake Azam.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa straika huyo amekidhi vigezo vyote anavyovitaka Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera na mabosi wamempa mkataba.
“Makambo yupo nchini tangu mwezi ulioisha, mwalimu amemwangalia kwa muda wote huo na kujiridhisha anafaa kuisaidia Yanga, ndio maana ameuambia uongozi umpe mkataba na tumetekeleza hilo kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili,” alisema bosi mmoja wa Yanga.
Mwanaspoti linafahamu kuwa kabla ya kusaini mkataba huo, Makambo alifanyiwa vipimo vya afya na kufuzu.
Katika hatua nyingine, Meneja Yanga, Hafidh Saleh, amesema kikosi cha timu hiyo kinatarajia kushuka dimbani leo Jumamosi kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania, uwanjani Uhuru.
“Mwalimu ameomba mchezo wa kirafiki ili kujaribu silaha zake kabla kukutana na Gor Mahia hivyo, tumewaomba JKT Tanzania na wamekubali,” alisema Hafidh.

No comments

Powered by Blogger.