Full-Width Version (true/false)


MOI kukata viungo majeruhi bodaboda sababu hiiTAASISI ya Mifupa Muhimbili (MOI), imeeleza sababu ya kuchukua uamuzi wa kuwakata miguu au mikono majeruhi wa ajali za pikipiki,  maarufu kama bodaboda.

Taasisi hiyo hupokea majeruhi wa ajali za pikipiki pekee 20 kila siku, huku ikilazimika kufanya upasuaji kwa majeruhi wa ajali mbalimbali 25 kila siku mbali na wagonjwa wa dharura.

Daktari Bingwa wa Mifupa Moi, Dk. Paul Kazungu, akizungumza na Nipashe jana katika banda la Moi, lililopo katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam, alisema hadi mgonjwa kufikia hatua ya kukatwa kiungo lazima iwe imethibitishwa na madaktari bingwa watatu.

Dk. Kazungu alisema sababu ya kwanza ni pale mgonjwa anapopata ajali na kubainika kuwa mfupa umesagika sana, jambo linaloweza kusababisha sumu kuingia kwenye mzunguko wa damu na kufanya figo kushindwa kufanya kazi.

Alitaja sababu ya pili kuwa ni mgonjwa kukatika mfupa wa fahamu na wa damu hali inayosababisha damu kushindwa kuzunguka na kupeleka kwenye mfumo wa fahamu.

Dk. Kazungu pia alisema endapo mshipa wa damu utakatika wenyewe, mgonjwa anaweza kukatwa kiungo, lakini wa fahamu ukikatika anaachwa kwa sababu hauna madhara kwenye fahamu isipokuwa anaweza kupooza mwili na kubaki na kiungo chake.

“Ipo dhana kuwa mgonjwa wa ajali ya pikipiki akifika Moi anaingizwa chumba maalum na kukatwa mguu au mkono moja kwa moja si kweli kabisa. Hadi mgonjwa akatwe kiungo chake lazima tuwe tumejiridhisha madaktari bingwa zaidi ya watatu, hivyo jamii inatakiwa kondokana na dhana hiyo potofu," alisema.

Dk. Kazungu alisema kutokana na kuwapo kwa dhana hiyo potofu wagonjwa wa ajali za pikipiki wamekuwa wakitoa taarifa za uongo.

“Kwa sababu jamii imepokea taarifa za uongo na kuziamini, majeruhi wa ajali ya pikipiki akija hospitali anadanganya kuwa kapata ajali wakati akikimbia shambani au vingine, lakini hasemi kama amepata ajali ya pikipiki akihofia kukatwa kiungo hali inayosababisha kutokuwa na taarifa sahihi za mgonjwa na kukosa takwimu kamili," alisema.

Dk. Kazungu aliitaka jamii kuondokana na dhana potofu ya kuamini kuwa wanakata watu viungo bila ya sababu za msingi.

Alisema hata hivyo takwimu za wagonjwa wanaokatwa viungo inapungua kwa sababu ya kuendelea kukua kwa teknolojia ya utoaji huduma za matibabu.

“Utafiti wa idadi ya wagonjwa wanaokatwa viungo kwa sababu nilizoeleza kwa ajili ya kuokoa uhai wao bado unafanyika hivyo zitatolewa baadaye, lakini wamepungua sana. Wodi ya wagonjwa 80 ya majeruhi unaweza kukuta hakuna mgonjwa hata mmoja aliyekatwa kiungo,” alisema Dk. Kazungu.

Katika maonyesho hayo yanayoendelea hadi Jumapili wiki hii badala ya Ijumaa kama ilivyopangwa awali, zaidi ya wagonjwa 75 wamefika katika banda la Moi kupata ushauri.

No comments

Powered by Blogger.