Full-Width Version (true/false)


Mshindi wa kwanza kitaifa matokeo kidato cha sita autamani udaktari
Mshindi wa kwanza kitaifa katika masomo ya sayansi kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Anthony Mulokozi amesema ndoto yake ni kuwa daktari.
Mulokozi (20) anatoka shule ya sekondari Mzumbe mkoani Morogoro amesema tangu alipoanza shule, alipenda masomo ya sayansi na ndoto yake ni kuwa daktari ili aweze kuwahudumia Watanzania wenye matatizo ya afya.
MCL Digital lilifanya mahojiano na mwanafunzi huyo nyumbani kwao mtaa wa Murutambikwa katika mji wa  Rulenge Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
 “Nilianza kupenda kuwa mtumishi wa afya ili kufuata nyayo za mama yangu ambaye ni muuguzi. Nilipenda zaidi masomo haya kwa sababu ya motisha iliyotolewa na pia nilifanya vyema katika matokeo ya darasa la saba,” amesema.
“Nilishika namba moja katika wilaya ya Ngara na kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana na Tabora.”
Amesema katika matokeo ya kidato cha nne alipata daraja la kwanza, katika mitihani ya ndani ya kidato cha sita katika shule ya Mzumbe, kati ya wanafunzi 121 alikuwa akishika namba tatu hadi ya kwanza.
“Natamani nikianza chuo kikuu nipate nafasi ya kwenda nje ya nchi kujifunza zaidi uchunguzi wa kisayansi kuhusu mwili wa binadamu,” amesema.
Mulokozi amezaliwa Juni 14, 1998, alianza elimu ya msingi mwaka 2005 hadi 2011 katika shule ya Rhec na baadaye kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana ya Tabora kuanzia mwaka 2012 hadi 2016.
“Baada ya hapo, kidato cha tano na sita nilisoma Mzumbe nikichukua mchepuo wa PCB (fizikia, kemia na baiolojia),” amesema.
Mwalimu wa shule ya msingi Rhec, Helena Adrian amesema kijana huyo alikuwa akipenda kujifunza na alikuwa akishika nafasi ya kwanza au ya pili.
“Ni kijana wa kuigwa kwa kweli. Amelelewa katika mazingira ya kumcha Mungu. Alikuwa akipenda udadisi na kufanya uchunguzi wa kisayansi, alikuwa mwanafunzi bora anayejituma,” amesema Helena.
Wazazi wa Mulokozi,  Julius Kalugendo na Angella wameieleza MCL Digital kufurahishwa na matokeo ya mtoto wao, kubainisha kuwa ni matunda ya usikivu wake kwa kila alichoelezwa.
“Tuna watoto wanne, Anthony ni wa tatu kuzaliwa. Kwa kweli alikuwa akipenda sana masomo ya sayansi. Kama familia kipato chetu kinatokana na shughuli za kilimo na ufugaji, tulijibana kuhakikisha watoto wanapata elimu nzuri,” amesema Angella.
Kwa upande wake Kalugendo amesema alikuwa akijua kuwa Mulokozi atafanya vyema katika masomo yake kwa kuwa alifanya vizuri katika mtihani wa kujiunga na shule ya seminari.
“Nakumbuka mapadri walimuita akajiunge na shule hizo lakini yeye hakupenda akaenda kusoma shule ya Serikali. Walimpenda kwa kuwa ni mnyenyekevu.  Nawashukuru waliomsaidia mtoto wangu katika masomo yake na imani yake, hata yeye nampongeza kwa kushirikiana na wenzake,” amesela Kalugendo.
Kalugendo ni ofisa mifugo kata ya Rulenge wilayani Ngara akijihusisha na ufugaji wa kuku wa mayai,  mama yake ni muuguzi msaidizi wa hospitali ya Rulenge.

No comments

Powered by Blogger.