Nyota waliopaishwa na kombe LA Dunia

Kutoka kushoto ni Hirving Lozano wa Mexico, Aleksandr Golovin wa Urusi na Juan Quintero wa Colombia.
Katika fainali za kombe la dunia mara
zote huwa vinapatikana vipaji vipya ambavyo hupata nafasi ya kusajiliwa
na klabu kubwa. Moja ya mifano ni James Rodriquez ambaye alisajiliwa na
Real Madrid kutoka Monaco baada ya kufanya vizuri kwenye fainali za
mwaka 2014.
Kwa mujibu wa wachambuzi mbalimbali wa
soka duniani, fainali za mwaka huu hazijatoa vipaji vipya vya kuonekana
moja kwa moja lakini kuna vipaji ambavyo vinaonekana kunufaika kutokana
na viwango walivyoonesha na inaweza isiwe tabu kwa mawakala wao kuwauza
kwenye timu kubwa.
1. Hirving Lozano, huyu ni nyota wa PSV
Eindhoven ambaye ameonesha kiwango bora akiwa na Mexico. Ana miaka 22 na
wakala wake ni Mino Raiola, ambaye ameripotiwa kuwa kwenye mazungumzo
na klabu za Arsenal, Barcelona na Manchester United kukamilisha uhamisho
wa nyota huyo.
2. Aleksandr Golovin, raia wa Urusi
ambao walikuwa wenyeji wa fainali na kutokana na kiwango chake
aliisaidia timu yake kufika hatua ya robo fainali. Anachezea CSKA Moscow
na klabu ya Chelsea imeripotiwa kuhitaji huduma yake.
3. Wilmar Barrios na Yerry Mina, hawa ni
nyota wa Colombia, Wilmar akicheza kiungo na Mina beki wameonesha ubora
mkubwa na pengine kwa Mina kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha
Barcelona huku Wilmar (24) anayechezea Boca Junior ya Argentina
akivivutia vilabu vya Tottenham na PSG.

Kutoka kushoto ni Yerry Mina wa Colombia, Jo Hyeon-Woo wa Korea Kusini na Alireza Jahanbakhsh wa Iran.
4. Juan Quintero, huyu ni nyota mwingine
wa Colombia anayechezea River Plate ya Argentina, ana miaka 25 na
ameonesha kiwango kikubwa na sasa anatajwa kuwaniwa na klabu ya Real
Madrid pamoja na Tottenham.
5. Alireza Jahanbakhsh na Milad
Mohammadi, hawa ni nyota wa Iran ambao walilisaidia taifa hilo
kuwashangaza wengi kwa kutoa upinzani mkubwa kwa timu za Hispania na
Ureno katika kundi B. Alireza (24) ambaye ni winga wa AZ Alkmaar sasa
anawindwa na vilabu vya Leicester City na AC Milan. Mlinzi Milad (24)
yeye anatajwa kuhitajika na klabu za Celtic na Rangers.
6. Jo Hyeon-Woo, huyu ni mlinda mlango
wa Japan anayechezea timu ya Daegu FC, kutokana na kiwango chake
alichoonesha kwenye mechi za kundi F sasa anatajwa kuwaniwa na
Liverpool.
Hao ni baadhi tu ya nyota ambao
wanatajwa sana kwenye dirisha la usajili kutokana na viwango vyao kwenye
kombe la dunia 2018, ambalo limemalizika Julai 15 kwa Ufaransa
kuwafunga Croatia mabao 4-2 na kuibuka mabingwa.
No comments