Full-Width Version (true/false)


Rasta mpya Yanga kazikazi tu!
YANGA imeanza fujo zake za usajili bana. Hadi sasa imesajili wachezaji watatu kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara. Usajili huu ni baada ya kuwa kimya tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa huku watani zao Simba na Azam wakifanya vurugu mapema wakinyakua huyu na yule kwa mikogo. Nyota waliosajiliwa Yanga mpaka sasa ni viungo watupu, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ aliyetokea Mtibwa Sugar, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka JKU ya Zanzibar na Jafary Mohammed ‘Rasta’ wa Majimaji ya Songea ambayo imeshuka daraja. Yanga mara baada ya kukamilisha usajili wa viungo hao waliwatambulisha kwa mashabiki wao pale Makao Makuu, Jangwani.
Mwanaspoti ilifanya mahojiano na Mohammed ‘Rasta’ ambaye kabla ya kutua Yanga alikuwa akiwindwa na KMC ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu, Mbao na Mwadui ambao wote walimkosa.
ANA MZUKA USIPIME
Rasta huyo ameonyesha kuwa na mzuka kinoma wa kuanza kazi kwenye kikosi cha Yanga chini ya kocha Mkongomani Mwinyi Zahera, ambaye kabla ya kusainishwa mkataba alifanya mazoezi ili kumuona kiwango chake.
Anasema Zahera alimuona katika mazoezi yaliyofanyika uwanja wa Chuo cha Polisi College Kurasini na kumpitisha bila kupinga kuwa anastahili kucheza Yanga.
“Natamani kwenda kuanza kazi haraka ili kuzoea mazingira yote ya timu na kufanya kazi ile ambayo Yanga waliona kutoka kwangu, naamini nina uwezo wa kuisadia timu kufikia malengo yake,”
“Naomba Mungu anipe nguvu na afya njema ili kuanza kazi yangu na kutimiza yale ambayo nimeyapanga hapa Yanga ingawa ni mapema kuyasema lakini mimi kama binadamu mwingine nina malengo,” anasema.
ZAHERA NOMA
Mohammed alifunguka zaidi kwamba katika majaribio aliyofanya siku ya kwanza chini ya Zahera na kumtamkia wazi kwamba anauwezo wa kucheza Yanga na kuisadia timu basi maneno hayo bado yapo akilini mwake.
“Maneno yake bado yapo akilini mwangu, natakiwa kujituma nikiwa mazoezini hata kwenye mechi ili kufanya kila jambo ambalo atakuwa anahitaji na kutojutia kunisajili ili aendelee kuniamini.
“Naamini nikiweza kufanya hivyo nitaendelea kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Zahera,” anasema Mohammed.
KAMUSOKO, BUSWITA WAJIANDAE
Alisema katika kikosi hicho kuna viungo wengi wazoefu, Papy Kabamba Tshishimbi, Thaban Kamusoko na Pius Buswita na wengine lakini amejiandaa kupambana nao.
“Katika maisha ili ufanikiwe ni lazima ukubali kukutana na changamoto na kama ukizishinda basi hata maisha unaweza kufanikiwa na kufikia yale malengo. Hiyo ndio changamoto yangu ya kwanza kuwakuta wachezaji wazoefu hapa Yanga lakini nimejipanga kujituma, kufanya mazoezi ya kutosha na kutumia vizuri nafasi yoyote nitakayopata bila kusahau nidhamu ya hali ya juu.
“Nikiyafanya hayo naweza kushindana na kupata nafasi hiyo licha ya kuwepo viungo hao ambao wamekuwa wakizoeleka kucheza lakini natambua uwezo wao ni mkubwa na nawaheshimu pia,” alisema.
FUNDI WA PASI
Mohammed tangu akicheza Toto Africans misimu miwili iliyopita alikuwa ni fundi wa kupiga pasi ndefu na fupi na katika kila mechi mara nyingi lazima atatangeneza nafasi ya madhara kwa wapinzani.
Uhodari huo aliuhamishia katika klabu ya Majimaji ambayo alisaini mkataba wa mwaka mmoja na kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza kutegemewa licha ya kushindwa kuisadia timu hiyo kubaki Ligi Kuu.
Katika kitu ambacho anajivunia ni kupiga pasi ndefu na fupi na akipata muda wa kucheza na kuzoana na wachezaji wenzake basi atafanya vizuri zaidi.
“Kubwa ni ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu jambo ambalo naamini halitashindikana lakini ninachotaka kuwaambia wana Yanga kila nilichokifanya nyuma nitakionyesha hapa zaidi,” alisema
NGASSA ATAFURAHI
Uhodari huo wa kupiga pasi ndefu utakuwa na faida kwa Mrisho Ngassa kama kweli viongozi wa Yanga watakuwa wamemalizana na winga huyo mwenye uwezo wa kukimbia akiwa anatokea pembeni.
Ngassa ambaye anasifika kwa mbio na kwa jinsi ambavyo Mohammed anaweza kupiga pasi ndefu basi muda wote atakuwa akiwasumbua mabeki wa timu pinzani kila watakapokutana nao.
“Kweli kabisa hata ukiangalia wakati nipo Majimaji msimu uliopita nilikuwa napiga pasi hizo kwa washambuliaji kama Marcel Kaheza na kama atakuwepo mchezaji wa aina hiyo hapa sitaacha kufanya hivyo kwani hiyo ndio kazi yangu na ndicho kilichonileta hapa,”
“Nadhani jukumu hilo litabaki kwa kocha kama nitaendelea kufanya jambo hilo muda mwingine kuna walimu hawapendi pasi ndefu wanataka fupi fupi hata hizo nipo vizuri pia,” anasema.
YANGA KAMA NJIA
“Kuja Yanga ilikuwa ni moja ya malengo yangu, nashukuru nimefanikiwa, lakini malengo mengine lazima niwe nayo na kubwa kufikilia kucheza mbele zaidi ya hapa, naamini Yanga itakuwa kama njia kwangu kwenda kucheza soka zaidi na siyo kurudi nyuma yaani timu ya chini ya Yanga, nikifanya vizuri zaidi naweza kupata nafasi ya kucheza timu ya taifa.
KUMBE NI KIRAKA
Yanga hawajafanya usajili wa Mohamed kwa lengo moja. Mohamed pia ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya mbili, beki wa kushoto, kiungo mkabaji na mshambuliaji na namba kumi, kwa sifa hizo huanda akawa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha Yanga.
“Kweli naweza kucheza katika nafasi hizo zote na nimesajiliwa hapa kama kiungo lakini huwezi jua pengine mwalimu anaweza kunichezesha kama beki wa kushoto au mkabaji na hata namba kumi yote yanawezekana,” alisema.

No comments

Powered by Blogger.