Full-Width Version (true/false)


Sababu tatu zinazoipa Ufaransa ubingwa Kombe la Dunia

 

Moscow, Russia. Hatimaye mtanange uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu umefika. Leo Ulinwengu wa soka utashuhudia historia ikiwekwa Russia.
Wapenda soka wanajiandaa kushuhudia kisasi kikilipwa. Muda mfupi ujao, takribani masaa 12 zijayo, tutajua mbivu na mbichi. Ufaransa Vs Croatia, patachimbika!

Kuelekea mchezo huu, baada ya kuangaliza sababu tatu ambazo zinaweza kuibeba Croatia dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa leo tunaigeukia Les Blues na kuangazia sababu tatu ambazo zinaweza kuwapa ushindi dhidi ya Croatia pale Luzhniki kuanzia saa 12 jioni.

1. Mshikamano na Uimara wa kikosi
Kama kuna kikosi kilichoonyesha mshikamano mkubwa basi ni Les Blues. Kuanzia mchezo wao wa kwanza, Ufaransa wamekuwa na mshikamano mkubwa, sio safu ya beki, kiungo au ushambuliaji. Takwimu zinajieleza zenyewe.
Kuanzia mechi ya kwanza, Les Blues wametanguliwa na timu pinzani katika dakika tisa tu. Kiungo wao Ngolo Kante amepokonya mipira mara 48, Hugo Lloris amechomoa michomo saba, huku wakipata ushindi katika mechi nane kati ya mechi 11 alizosimama langoni.

2. Morali ya Timu
“Mechi za Kombe la Dunia haziheshimu kiwango binafsi ya mchezaji bali timu. Kama mtacheza kama timu, ni rahisi kushinda kuliko kutegemea kiwango cha mtu mmoja mmoja." Hiyo ni kwa mujibu wa Kocha wa Ubelgiji, Mhispania Roberto Martinez. Ushahidi wa kauli ya Martinez, kipo kwa vijana wa Didier Deschamps.

Licha ya kuwa na mastaa kama Antoine Griezmann, Hugo Lloris, Kylian Mbappe, Olivier Giroud, Paul Pogba, Rafael Varane na Blaise Matuidi, Les Blues wamekuwa wakicheza kwa mshikamano, wakitegemeana na ndio maana sio ajabu kusikia Giroud hafungi lakini anaokoa hatari, anakaba na kupiga pasi za mabao.

3. Historia inawabeba
Miaka 20 baada ya kuiongoza Ufaransa kuipiga Croatia ya kina Davor Suker, Slavec Bilic, Niko Kovac na Antony Seric, Didier Deschamps amekutana tena na watoto wa mama, akiwa kikosi cha Nyota kadhaa wanaotamba Ulaya, lengo lake likiwa ni kuendeleza ubabe.

Kama Ufaransa watashinda mechi hiyo, Deschamps ataweka rekodi akiungana na Mario Zagallo (Brazil) na Franz Beckenbauer (Ujerumani) katika orodha ya makocha waliotwa kombe hili wakiwa manahodha na kocha. Hapa ndipo ugumu wa mechi hii unapoanzia.
Nani hataki kuweka rekodi?

No comments

Powered by Blogger.