Full-Width Version (true/false)


Serikali yawapa angalizo wananchiSerikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wananchi kutoa taarifa kwa hospitali, zahanati au kituo cha afya chochote kitakachokuwa kinatoa majibu ya kipimo cha typhoid ndani ya nusu saa kwa kuwa siyo utaratibu za kitabibu.

Tamko hilo limetolewa na Naibu wa Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile wakati akizungumza na eatv.tv leo Julai 10, 2018 baada ya kupita siku kadhaa tokea alivyotoa kauli yake iliyozua taharuki na kuwaacha wengi njia panda kuwa 'asilimia 70 ya homa Tanzania siyo malaria wala siyo typhoid, hivyo unapokwenda kwenye vituo vya afya kupimwa halafu ukaambiwa una typhoid inabidi uhoji ni kigezo gani kilichotumika mpaka uambiwe unaumwa ugonjwa huo'.

"Mara nyingi sana katika vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya kumekuwa na tatizo la kila mgonjwa kuwa na malaria au muda mwingine kusema ana typhoid. Utaratibu wa kupima kipimo cha Typhoid sio kama wanavyosema kuwa unaenda leo unapimwa halafu unapatiwa majibu ndani ya nusu saa. Mara nyingi kipimo hiki huwa kinatoa majibu ndani ya saa 48", amesema Dkt.Ndugulile.

Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile ameendelea kwa kusema "siasa na afya ni vitu viwili tofauti hivyo nawaomba wananchi wasipuuzie suala hili la kuhoji endapo watapewa majibu ya typhoid ndani ya nusu saa maana hiyo ni haki yao ya msingi".

Kwa upande mwingine, Naibu wa Waziri Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa mtu yoyote ambaye atalalamika kutopewa haki za msingi anapokuwa amekwenda hospitalini, anayohaki ya kwenda kufungua mashitaka na mtoa huduma kuchukuliwa hatua stahiki.

No comments

Powered by Blogger.