Full-Width Version (true/false)


Tani 95 za Chakula na Tani moja ya dawa zaangamizwa
Jumla ya Tani 95 za chakula na Tani moja ya dawa zimeangamizwa kutokana na kuharibika baada ya kuhifadhiwa kwa muda mrefu katika maghala yasiyo rasmi na yaliyokosa sifa za kutumika kwa kazi ya uhifadhi wa  vitu vya chakula na dawa.

Bidhaa ambazo zilizokuaghamizwa katika jaa la Kibele mkoa kusini unguja zilikuwa mchele tani 52, unga wa sembe tani sita , unga wa ngano tani 37 pamoja na Tani moja ya dawa za binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Usalama wa chakula Zanzibar  ZFDA Dkt. Khamis Ali Omar alisema bidhaa za chakula zilizoangamizwa za mfanyabiashara Mohamed Mattar ziliharibika baada ya kuhifadhiwa kwa muda mrefu katika maghala yasiyorasmi na yaliyokosa sifa za kutumika kwa kazi hiyo.


Aidha alisema Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imejidhatiti kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini zinawafikia wananchi zikiwa salama kwa matumizi kwa lengo la kulinda afya zao.

Dkt. Khamis alieleza kuwa kutokana na maghala hayo kukosa viwango vinavyokubalika na kutosajiliwa na ZFDA, mfanyabiashara Mattar alikuwa  akiweka bidhaa zake kwa siri wakati wa usiku.


Alisema sehemu ya bidhaa hizo zilikuwa zikitolewa kama sadaka katika mwezi wa Ramadhani kama mbinu ya mfanyabiashara huyo kujaribu kukwepa gharama za kuangamiziwa bidhaa zake.

Mkurugenzi Idara ya Udhibiti na Usalama wa Chakula aliwataka wafanyabiashara wanapotaka kutoa sadaka ya chakula kuishirikisha ZFDA ili kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa itakayotolewa.

Mfamasia wa ZFDA Nassir Buheti alisema kiwango kikubwa cha dawa zilizomaliza muda wa matumizi zilitoka Taasisi za kiraia (NGO) kwa ajili ya kuangamizwa  na kiwango kidogo kilipatikana katika maduka ya kuuzia dawa.

Buheti alitoa wito kwa maafisa wa NGO wanaopata msaada wa dawa kutoka nje kuwa waangalifu katika kuzitumia na inapokaribia miezi mitatu kabla ya kumaliza muda wa matumizi na wakihisi haziwezi kumalizika wazipeleka ZFDA ili wazisambaza katika vituo vya afya vya Serikali ambako mahitaji ya dawa ni makubwa.


No comments

Powered by Blogger.