Full-Width Version (true/false)


Taulo za kike zinazofuliwa zasambazwa shuleniMBUNGE wa Longido, Dk. Steven Kiruswa na mkewe Agnes, kwa kushirikiana na rafiki yao raia wa Marekani, Sarah Messenger, wamegawa taulo za kike 400 zinazofuliwa na kutumika tena kwa wanafunzi wa shule nane za msingi na sekondari wilayani. 

Hatua hiyo imeelezwa ni ya kuwaondoa wanafunzi wanaotoka kaya duni katika adha ya kushindwa kuhudhuria shuleni na kukosa masomo pindi wanapokuwa katika siku za hedhi. Akizungumza katika hafla ya kukabidhi taulo hizo, Kiruswa alisema msaada huo umetolewa kwa jamii ambayo ina uhitaji mkubwa kutokana na kuwa na kipato cha chini kumudu gharama za taulo hizo. 

Alisema zimetolewa muda mwafaka ambapo, Julai mosi mwaka huu Bunge lilipitisha azimio la kuondoa kodi kwa taulo za kike. 

Mapema Sarah alisema, baada ya kurudi nyumbani na kuzungumza na wanawake wenzake wa Jimbo la Michigan walikubali na kufanya harambee maeneo mbalimbali ikiwamo shuleni na makanisani na kupata fedha za kununulia zana za kutengenezea na wakaanza utaratibu wa kukutana kila Jumatano jioni, kufanya kazi ya kushona taulo hizo katika vikundi vyao mbalimbali. 

Alisema kiasi hicho cha taulo zilizotolewa ni kama kwa majaribio, lakini iwapo zitaonyesha ufanisi na kuwafaa watoto hao wataleta zingine hadi pale itakapoonekana mahitaji yamejitosheleza na kuwa na ziada za kutosha kwa wanafunzi wa shule zote wilayani humo. 

Akifafanua kuhusu taulo hizo, alisema kipo kivalishio kimoja ambacho huweza kutumiwa hadi siku za hedhi zitakapomalizika, ambapo kivalishio hicho kinakuwa na taulo nne ambazo moja ikichafuka inabadilishwa na nyingine kufuliwa. 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mhina alisema msaada huo ni wa maana kubwa na taulo hizo ndizo zinazofaa kulingana na mazingira hayo kwa kuwa ni kweli mahudhurio ya wanafunzi wa kike katika kila mwezi shule zote yalikuwa si mazuri kutokana na kushindwa kumudu gharama za manunuzi ya taulo zile zisizofaa kutumika na kurudiwa. 

Alisema kwa msaada huu wa taulo zinazotumika na kufuliwa kisha kurudiwa tena utawezesha wanafunzi hao wa kike kuhudhuria masomo bila kupata usumbufu. Hata hivyo, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia usafi kufua taulo hizo kabla ya kuzitumia kwa mara nyingine. 

Akitaja shule zilizonufaika na msaada huo wa mke mbunge huyo Agnes, alisema ni Longido Shule ya Msingi na Sekondari, Shule ya Msingi Olbomba, Shule ya Msingi Kimokouwa, Shule ya Msingi Oriendeki, Shule ya Msingi Engarnaibor, Shule ya Sekondari Engarnaibor na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lekule. 

Alisema msaada kama huo alishawahi kuutoa miaka miwili iliyopita ingawa hakufanikiwa kufikia shule zote, lakini kwa sasa kupitia rafiki yake huyo na wenzake walioko Marekani pamoja na hapa nchini na kwamba mpango huo ni endelevu, ili kumkwamua kielimu mtoto wa kike wa jamii hiyo ya kifugaji.

No comments

Powered by Blogger.