Full-Width Version (true/false)


Tuzo Mchezaji bora Kombe la Dunia pasua kichwa

 

Moscow, Russia. Hatimaye mchezo uliosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka, wa fainali za Kombe la Dunia 2018 unatarajiwa kupigwa kesho kati ya Ufaransa na Croatia.

Katika mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Luzhniki, Moscow, sio tu utampata bingwa wa Dunia, lakini ndio unaotarajiwa pia kumtangaza mchezaji atakayetwaa tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la Dunia.

Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa na nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo ni nahodha wa Croatia, Luka Modric na kiungo mkabaji wa Ufaransa, N’golo Kante.

Tuzo hiyo mwaka 2002 ilitwaliwa na mshambuliaji mahiri wa Brazil, Ronaldo Nazario de Lima, 2006 ikatwaliwa na nahodha wa Ufaransa, Zinedine Zidane, 2010 ikatwaliwa na mshambuliaji wa Uruguay, Diego Forlan na 2014 Lionel Messi, akaitwaa tuzo hiyo.

Ingawa kwa kanuni za Fifa sio lazima mchezaji bora wa mwaka atokane na timu iliyotwaa ubingwa wa Dunia, lakini Luka Modric na N’Golo Kante, wanapewa nafasi kubwa kutokana na mchango wao binafsi ulioziwezesha timu zao kufika fainali.

Wote wawili wameziwezesha timu zao kufika fainali, Modric akiingiza Croatia fainali ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, Kante naye anaonekana kukaribia kuipa Ufaransa taji la pili la ubingwa wa Dunia.

Mbali ya Modric na N’Golo Kante, pia mshambuliaji kinda wa Ufaransa, Kylian Mbappe na kiungo Paul Pogba, wanayo nafasi ya kutwaa tuzo hiyo kutokana na kung’ara kwao.

Pia Antoine Griezmann wa Ufaransa, Ivan Perisic, Mario Mandzukic na Ivan Rakitic wa Croatia, wanayo nafasi ya kutwaa tuzo hiyo.

No comments

Powered by Blogger.