Full-Width Version (true/false)


Ufaransa Vs Croatia ni zaidi ya fainali, ni mechi ya Heshima, Ubabe na Kisasi

 

Moscow, Russia. Zimesalia takribani saa 24 tu, tuelekee Luzhniki kushuhudia historia ikiandikwa katika ardhi ya Warusi. Itakuwa ni mechi ya ubabe na kisasi. Itakuwa ni vita vya heshima. Vitakuwa ni vita vya mafahali wawili kutoka Ulaya.

Majira ya saa 12 jioni, mji wa Moscow utafurika. Uwanja wa Luzhniki utakuwa mwenyeji wa mashabiki 81,000. Vibanda umiza, hasa kwa masai muuza kahawa, vitajaa pomoni. Wenzangu wa kubeti, mbona mikeka ishatandikwa tu. Croatia Vs Ufaransa ndio habari mjini.

Julai 15, itakuwa ni siku kukumbukwa katika kalenda ya FIFA. Mmoja kati ya Ufaransa na Croatia ataenda nyumbani akicheka.
Sijui ni nani ila ninachokifahamu ni kwamba, huu utakuwa ni muendelezo wa mechi ya nusu fainali ya 1998. Luca Modric na wenzake watawalipia Davor Suker na wenzao kisasi cha kupigwa 2-1?

Je, Paul Pogba, N'Golo Kante, Kylian Mbappe, Antoine Griezmann, Olivier Giroud na Blaise Matuidi, wataendeleza ubabe wa Ufaransa dhidi ya watoto wa mama? Jibu la hili swali tutalipata baada ya dakika 90, kukamilika kwenye dimba la taifa la Russia, wenyewe wanaliita Uwanja Luzhniki.

Tuachane na hayo kwa sasa. Kuelekea mtanange huu, kuna kitu ambacho wengi hawaufahamu. Ni kwamba, mechi hii itakuwa ni zaidi ya fainali.

Ukiangalia vikosi vya timu hizi, utagundua kuwa, kuna vita nyingine itakayoshuhudiwa pale Luzhniki. Kutakuwa na vita ya nani mkali.
Swali la kujiuliza ni Je, N'Golo Kante ataweza kumzuia Luka Modric kufanya mambo yake pale kati? Je, Croatia wana ubavu wa kumzuia Kylian Mbappe, kuleta madhara akitokea Winga ya kulia? Vipi kuhusu Ivan Perisic, Les Blues watamuweza? Mwanaspoti inakuchambulia kwa makini

KANTE VS MODRIC
Katika mechi ya kesho kutakuwa na mpambano mkali katikati ya dimba la Luzhniki kati ya kiungo wa Chelsea NG'olo Kante na kiungo wa Real Madrid, Luca Modric. wawili hawa mpaka sasa ndio viungo walioonyesha kiwango bora zaidi na sasa watachuana kuweka heshima na kuondoa ubishi ya nani mkali kati yao. unadhani nani atashinda vita hii?

Kante amekuwa silaha muhimu kwa Les Blues kuzima juhudi za wapinzani akizunguka uwanja mzima huku Modric ambaye ni nahodha wa Croatia, amekuwa kamanda wao na kete ya mwisho kusaka ushindi, mara nyingi akikimbia nyuma ya Mario Manzukic, Ivan Perisic na Ivan Rakitic.

Kama kuna mtu ambaye Ufaransa watamtumia kumuweka Modric mfukoni, basi ni Kante, kama walivyofanya katika mchezo dhidi ya Ubelgiji walipomficha Eden Hazard. mpaka sasa, Croatia wana rekodi ya kutawala mechi tano kati ya sita, huku Ufaransa wao wanajivunia kutawala kila mechi.

MBAPPE V PIVARIC
Kutakuwa na shughuli pevu kati ya Kylian Mbappe na Pivaric katika winga ya kulia. kumbukumbu ya hatari wa Mbappe, unaturudisha katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ubelgiji ambapo ilimchukua sekunde 14 kumuonesha Jan Vertonghen yeye ni nani.

Akitumia kasi yake, Mbappe alimuacha beki huyo wa Tottenham akihema kabla ya kuachia pasi ya kimo cha mbuzi, kuelekea katika boksi ya Ubelgiji. Akarajea tena na kumlamba chenga hatari kabla ya kuachiza krosi nyingine. unakumbuka alivyompiga tobo?

Kazi hii anakabidhiwa Josip Pivaric, mwenye umri wa miaka 29. Pivaric atakuwa na kibarua cha kumkaba Mbappe mwenye umri wa miaka 19, unaona maajabu ya soka? kinachoweza kumkuta Pivaric hakina tofauti na kilichowakuta mabeki wa Argentina na Ubelgiji.

VARANE V MANDZUKIC
Wala hawana shida. Safu yao ya kushambulia iko fiti kalikiti. Pale mbele yupo mzee mzima, Mario Mandzukic na mauzoefu kibao. Katika michuano hii, muuaji huyo aliyeitoa roho ya England, katika dakika za lala salama amekuwa moto wa kuotea mbali. Ana hasira balaa. Akikosa goli ujue Ivan Perisic au Ivan Rakitic hawakuachi.

Hata hivyo, katika mechi ya kesho, kutakuwa na shughuli kubwa kati ya Mandzukic na Rafael Varane. Niamini mimi, patachimbika kati ya wawili hawa. Aliwatungua Denmark katika hatua ya mtoano kabla ya kuwazika wajukuu wa Malkia.

Lakini dhidi ya beki wa Real Madrid, Raphael Varane, mbona atapata tabu sana. Varane hanaga mchezo kazini, lakini wakati huo huo, Mandzukic mtata kama lilivyo jina lake, kutakuwa na vita ya Dunia.

Wawili hao wameshakutana mara nyingi sana, ukianza na mechi ya nusu fainali ya pili ambapo Mandzukic, alimpita Varane mara mbili akiitungua Los Blancos.

No comments

Powered by Blogger.