Full-Width Version (true/false)


Ushauri wa Pinda kwa ATCLWAZIRI MKUU MSTAAFU, MIZENGO PINDA.

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amelishauri Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kufanya kazi kwa pamoja na Bodi ya Utalii (TTB), ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini.

Amesema TTB na ATCL zinategemeana katika utendaji wa kazi, hivyo lazima zifanye kazi kama timu.

Pinda aliyasema hayo jana alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa.

Alisema taasisi hizo zikishirikiana kikamilifu zitachochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kwa kutumia ndege za ATCL.

"Kwa sasa tuna usafiri wa uhakika tofauti na mwanzo, hivyo ni lazima tuone mabadiliko kwenye sekta ya utalii," alisema Pinda.

Aliwahakikishia kuwa endapo watafanya kazi kwa umoja watafikia malengo makubwa na kusababisha nchi kuwa na uchumi wa kati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladsilaus Matindi, alisema hadi  sasa wamekuwa na utaratibu wa kukutana na TTB mara mbili kwa wiki, ili kujadiliana na kupanga mikakati ya maendeleo baina yao.

Alisema kwa sasa wameshapiga hatua kubwa kutokana na vikao ambavyo wamekuwa wakikutana na kwamba matokeo yameanza kuonekana.

Matindi alimhakikishia Pinda kuwa ujio wa ndege mpya waliyoipokea hivi karibuni aina Boeing 787-8 Dreamliner, utachangia kuifungua Tanzania katika nyanja za kiuchumi kwa kuleta watalii wengi zaidi nchini.

No comments

Powered by Blogger.