Full-Width Version (true/false)


Usibishe! Umemjua Rais wa Croatia kupitia Kombe la Dunia

                 Moscow, Russia. Jina la Kolinda Grabar limeingia katika orodha ya majina maarufu yaliyochomoza katika Fainali za Kombe la Dunia.

Kolinda amepata umaarufu na dunia imemtambua kutokana na aina ya uhamasishaji wake katika fainali hizo zilizochezwa nchini Russia.

Rais huyo wa Croatia ameacha gumzo katika fainali hizo baada ya kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wachezaji wa timu hiyo akipiga kambi nchini Russia.

Mbali na akina Luka Modric, Ivan Rakitic, Ivan Perisic au mkongwe Mario Mandzukic, Kolinda hakuwa mtu wa mchezo katika fainali za mwaka huu.

Croatia iliandika historia kwa kucheza fainali ya Kombe la Dunia licha ya kufungwa mabao 4-2 na Ufaransa.

Rais Kolinda alikuwa mmoja wa marais watatu waliopewa heshima na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kusimama mbele ya jukwaa kuu kutoa zawadi kwa washindi mbalimbali, akiungana na Emmanuel Macron wa Ufaransa na Vladimir Putin kutoka Russia.

Kolinda mwenye miaka 50, aliyeingia madarakani Februari 19, 2015, alisimama kidete bila kujali mvua katika siku ya fainali ambapo alishiriki hadi mwisho katika kazi ya kutoa medali kwa wachezaji wa timu zote mbili.

Alionyesha ujasiri wa hali ya juu kwanza kwa kustahimili mvua na pili kwa kufungwa nchi yake, tukio hili la baada ya mchezo wa fainali limekua likiwekwa kwenye mitandao mbali mbali ya kijamii duniani kote.

Baada ya Croatia kutinga fainali, Kolinda aliongoza kampeni kuhamasisha wananchi wote kuiunga mkono timu hiyo, akimtumia pia mwanamuziki mahiri Marko Perkovc.

Rais Kolinda amekuwa akiitangaza Croatia mbele ya viongozi wa mataifa mengine kwa mfano, aliwahi kuwapa jezi za timu yake ya Taifa, Kansela wa Ujerumani, Angela Mikel, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, Rais wa Marekani, Donald Trump na siku ya fainali alimkabidhi jezi Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Rais huyo aliwahamasisha wachezaji kupambana dakika 120 katika mechi zote za mtoano kuanzia ile ya 16 bora dhidi ya Denmark, robo fainali na Russia na nusu fainali dhidi ya England, kabla ya fainali kumalizika kwa dakika 90.

Kocha wa Croatia Zlatko Dalic, anamtaja Rais Kolinda ni kiongozi wa aina yake baada ya kuwahamasisha wachezaji wake kutetea Taifa lao.

Croatia ilianza kucheza mechi za kimataifa mwaka 1994 baada ya Taifa hilo kupata Uhuru, Juni 25, 1991 baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Yugoslavia.

Croatia Taifa lenye watu 4,154,200 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika Oktoba, 2017 ilitambulika duniani kutokana na kazi nzuri ya Rais Kolinda.

Kolinda ana watoto wawili na mumewe Jakov Kitarovic, anazungumza lugha za mataifa mbalimbali yakiwemo Croatia, England, Hispania, Ureno, Ujerumani, Ufaransa na Italia
 

No comments

Powered by Blogger.