Full-Width Version (true/false)


Wanaume wanaotoa talaka kwa ‘sms’ waonywaWAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Moudline Castico, amekemea tabia ya baadhi ya wanaume kuwataliki  kwa kutumia ujumbe wa simu. 

Akizungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi katika tawi la Kiembesamaki, Waziri Castico alisema kitendo cha kutaliki mke kwa staili hiyo ni dharau na udhalilishaji. 

Waziri huyo alisema baadhi ya wanaume wanaofanya hivyo, ni wale waliowezeshwa na wake zao wanaojituma, ambao hali za waume hao zilikuwa duni wakati wakioana. 

Alisema wapo wanaosaidiwa kujenga nyumba na hata kununuliwa magari na wake zao, lakini hatimaye wanawatoa thamani na kuwanyanyasa baada ya kupata wanawake wanaowaona ni wazuri zaidi. 

Alieleza kuwa, jambo baya zaidi ni kuacha kuwashughulikia watoto kwa kuwanyima huduma na matunzo, hali inayowasukuma kuzurura mitaani na kuingia katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji. 

Katika hatua nyingine imeelezwa kuwa vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto, vinaweza kukoma moja kwa moja iwapo kutakuwa na ushirikiano mzuri wa wazazi, walimu, viongozi wa dini na serikali. 

Hayo yameelezwa na Masheikh na Maimamu walioshiriki semina iliyoandaliwa na Ofisi ya Mufti kuhusiana na vitendo vya udhalilishaji. 

Akizungumza katika semina hiyo Shekhe, Rajam Muhammed alisema inasikitisha kuwa vitendo hivyo vinazidi kushamiri Zanzibar licha ya juhudi za serikali na taasisi binafsi kuongeza nguvu na kubuni mbinu mbalimbali ili kuvitokomeza. Walisema dawa ya kuondosha tatizo hilo ni kwa serikali na jamii kuwa tayari kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua kali watu wote wanaopatikana na hatia baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani. 

Aidha walisema vitendo vya ubakaji na ubaradhuli vinaonekana kuwa jambo la kawaida kwa kuwa jamii inaona aibu kuwataja wanaojishughulisha navyo. Akifungua semina hiyo, katibu wa Mufti Fadhil Suleiman Soraga, alisema vitendo vya udhalilishaji na ulawiti vinaipunguzia Zanzibar heshima yake mbele ya jamii ya kimataifa.

No comments

Powered by Blogger.