Full-Width Version (true/false)


Wandishi wa habari za mahakamani wapigwa msasaa
WAANDISHI wa Habari za Mahakama wametakiwa kufikisha habari fasaha kwa jamii inayowazunguka ipasavyo kwani wao ni nguzo muhimu katika kufikisha taarifa.


Hayo yamesemwa mapema leo Julai 16 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa-Morogoro, Mhe. Elizabeth Nyembele wakati alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo ya siku tano kuhusu Uandishi wa Habari za Mahakama.


Nyembele alisema kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na upotoshaji wa habari za Mahakama zinazotolewa na baadhi ya waandishi wa habari za Mahakama, aidha kwa makusudi au kutokujua sheria na taratibu za uandishi wa habari za kimahakama.

a
“Kupitia mafunzo haya, Mahakama inakusudia kuwapa Waandishi wa Habari mambo muhimu ya kuzingatia katika kuandika habari za Mahakama kwa jamii na hatimae kupunguza na kumaliza kabisa mkanganyiko wa habari za Mahakama,” alisema Mhe. Nyembele.


Mafunzo hayo ya siku tano (5) ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia yamelenga kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari za Mahakama ili waweze kuripoti vyema zaidi.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano-Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe alisema kuwa lengo la Mafunzo hayo ni kuwapa uelewa zaidi Waandishi wa Habari za Mahakama kupitia mada mbalimbali zitakazotolewa.


Nao waandishi wa Habari wanaoshiriki katika mafunzo wameisifu Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo wa kuripoti habari za Mahakama kwa ufasaha zaidi.


Mafunzo hayo yamehudhuriwa na jumla ya washiriki 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini zikiwemo Televisheni, redio, Magazeti na Blogu.


Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake imejiwekea nguzo kuu tatu moja ya nguzo hizo ni ya Ushirikishwaji wa Wadau. Kwa kuwajengea uwezo Waandishi wa habari za Mahakama, wananchi wataweza kupata taarifa nyingi na zilizo sahihi kuhusu utendaji kazi wa Mahakama.

No comments

Powered by Blogger.