Full-Width Version (true/false)


Waziri Mhagama Amtumbua Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajir


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,  Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Muhagama  ametengua uteuzi wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) Bw. Saneslaus Boniface Chandarua kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake wa kuisimamia Taasisi hiyo katika soko la ajira nchini.

Akizungumza na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika ukumbi wa Taasisi hiyo, jijini Dares Salaam tarehe 17 Julai, 2018, Mhe. Mhagama amesema amefikia maamuzi hayo kutokana Mtendaji Mkuu huyo kushindwa kuisimamia Taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi na utoaji wa huduma za ajira nchini kwa kuhakikisha kuwa Huduma za Ajira zinazotolewa kwa umma zinakuwa bora zaidi, zenye tija na zenye kuwafikia wananchi wengi zaidi, badala yake Taasisi hiyo imeendelea kufanya kazi kwa mazoea na Mtendaji Mkuu bila kuchukua hatua.

“Serikali inaitegema TAESA kuwa ni Taasisi ya kwanza kujua fursa ngapi zinazotengenezwa katika kila sekta iwe sekta ya umma au binafsi, ili kuweza kuzalisha soko la ajira kwa vijana wengi wanaomaliza masomo yao hata hivyo haifanyi kazi hiyo ipasavyo. Huku tukizingatia asilimia 56 ya nguvu kazi tuliyonayo ni vijana na wengi wako katika kautafuta ajira mbalimbali “ amesema Muhagama

Akifafanua baadhi ya mambo ambayo Mtendaji Mkuu huyo ameshindwa kuyasimamia vyema ni pamoja na kuunganisha watafuta kazi na waajiri, kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa ajira ndani na nje ya nchi, kukusanya, kufanya uchambuzi na kusambaza taarifa za soko la ajira kwa wadau na umma kwa ujumla na kushindwa kutambua fursa mbalimbali za ajira nchini na kuacha zikipita huku baadhi ya watendaji wa Taasisi hiyo wakijisahau kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo na Mtendaji mkuu bila kuchukua hatua.

“Serikali ya awamu ya tano inatekeleza miradi mingi ya maendeleo, ipo miradi ya ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, ujenzi wa stendi za kisasa na masoko makubwa, miradi ya maji, ujenzi wa hospitali, ujenzi wa Reli ya Kisasa, mradi wa Bomba la Mafuta toka Nchini Uganda, miradi ya kupeleka Umeme vijijini (REA) hapa nchini lakini mpaka sasa hamjaweza kubainisha fursa za ajira zitokanazo na miradi mingi kati ya hiyo na kuweza kuwaunganisha watafuta ajira, huo ni ufanyaji kazi wa mazoea,na haiendani na kasi ya serikali hii ” Amesema Mhe. Mhagama

Mhe. Waziri pia alionesha kutoridhishwa na utendaji wa Wasimamizi wa Kanda wa TaESA walio katika vituo mbalimbali nchini na kumtaka Kaimu Katibu Mkuu ambaye ni Kamishna wa Kazi kuwatathmini upya utendaji wao na kuwaondoa haraka ndani ya siku saba wale walioshindwa kutekeleza majukumu yao

“Inasikitisha kusikia msimamizi wa kanda anashindwa kufika katika maeneo yote ya Kanda yake kwa kusisitiza kuwa mtu huyo hawezi kujiita Msimamizi wa Kanda kama hatambui maeneo yote ya kanda yake. Mikoa hiyo ya kikanda imepangwa kimkakati na inafikika kiurahisi” amesema Mhagama.

Katika kuhakikisha Taasisi hiyo inafanya kazi kwa ufanisi Mhe Waziri ametoa maagizo matano kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Kamishna wa Kazi nchini na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu na maagizo hayo yanaanza kutekelezwa kuanzia sasa;

Agizo la kwanza ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ajira Bi.Kisa Kilindu kuhamia wizarani na Wafanyakazi wote wa TaESA wahamie mjini Dododma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira ), anatakiwa kufanya mabadiliko makubwa katika kuhamisha watumishi waliopo makao makuu ya Taasisi na wasimamizi wa kanda wote.

Kuwasilisha ofisini kwake taarifa za kila mwezi na robo mwaka juu ya utekekezaji wa majukumu ya TaESA na mpango kazi wa kila tukio ambapo Mhe. Waziri amesema atafuatilia kila hatua ya utekelezaji wake.

Kuanzia sasa amewataka TaESA kusitisha kazi ya kuwaunganisha Watafuta kazi nje ya Nchi isifanyike mpaka watakapokaa vikao kwa kushirikiana na Kamishna wa Kazi na wadau wengine na kuweka utaratibu sawa, pia kazi hiyo itafanyika kwa watanzania wenye ujuzi wa juu na ujuzi wa kati tu, na itakuwa kwenye nchi zilizokwisha ingia makubalianona na Tanzania (bilateral Agreements) .

Mhagama maemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira) na Menejimenti ya TaESA kuhakikisha kuwa wanavihusisha vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kuchunguza wale wote waliowahi kujihusisha, wanaoendelea na wanaotarajia kujihusisha na vitendo vya rushwa kuchukuliwa hatua haraka sana.

Ameagiza pia , Wakala Binafsi zitakazosajiliwa wawekewe utaratibu wa kuwa na kanzi data ya taarifa za watu watakaowaunganisha na kuwa na taarifa za huko wanakokwenda kufanya kazi na walete taarifa kamili za Mawakala wanaowaunganisha watanzania huko nje ya nchi.

Mhagama ameitaka TaESA kusimamia Wakala Binafsi wa Huduma za ajira ili watiize majukumu yao vizuri badala ya kuwa waajiri au kuwa sehemu ya mahusiano kati ya mwajiri na waajiriwa .

Kwa Mujibu wa Ibara ya Ibara 11 ya Mkataba wa Kimataifa Na. 88 wa mwaka 1948, unaohusu utoaji wa Huduma za Ajira, inaeeleza kuwa huduma za Wakala wa ajira zitatolewa bure kwa watafuta kazi hivyo TaESA wameagizwa kuzingatia hilo.

TaESA wanatakiwa kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao utakaoonyesha jinsi watakavyoshiriki katika kuelimisha vijana ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.

TaESA ni chombo kilichoanzishwa chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 (Executive Agencies Act) (kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009) na Tamko la Serilkali Na.189 la mwaka 2008 kutoka iliyokuwa

kituo cha Ajira Nchini (Labour Exchange Centre) iliyoanzishwa na Serikali. lengo la kuanzishwa kwa chombo hiki ni kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi na utoaji wa huduma za ajira nchini kwa kuhakikisha kuwa Huduma za Ajira zinazotolewa kwa umma zinakuwa bora zaidi, zenye tija na zenye kuwafikia wananchi wengi zaidi.

No comments

Powered by Blogger.