Waziri Mkuu Atoa Siku 14 Wajasiriamali Wahame......Ni baada ya kukagua eneo la viwanda vidogo na kupewa malalamiko
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama
Mji, Bw. Anderson Msumba ahakikishe ndani ya siku 14 anawahamisha
wajasiriamali wote waliogoma kuhamia eneo la viwanda la Bukondamoyo.
“Wauza
mbao, wachomeaji grili, wenye gereji wote, hakuna ruhusa kuendelea
kubakia mjini wakati tumewapa eneo la bure la ekari 500. Lile eneo ni
zuri kwa biashara lakini kuna watu wamegoma kuhamia kule. Mkurugenzi
hakikisha wote hawa wanahamia kule mara moja na atakayekiuka, akamatwe,”
alisema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati
akizungumza na wajasiriamali wachache waliohamia kwenye eneo la viwanda
la Bukondamoyo katika kata ya Zongomela, wilayani Kahama mkoani
Shinyanga mara baada ya kulikagua.
“Ninawaagiza
wajasiriamali wote walioko mjini wawe wamehamia huku ifikapo tarehe 30
Julai, 2018. Mkuu wa Mkoa ikifika tarehe moja Agosti, wewe njoo na
Kamati yako ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na mkiwakuta huko mjini,
wakamateni na kuwaweka ndani,” alisema.
Alimwagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama Mji aimarishe barabara za eneo hilo
kwa sababu kuna magari yanatakiwa kupeleka mizigo lakini pia kuna
magari ya wateja yatapaswa kwenda huko kwa hiyo ni lazima pafikike kwa
urahisi.
“Tengeneza
barabara, weka taa za barabarani za solar, lakini pia uangalie
uwezekano wa kuweka kituo kidogo cha polisi kwa sababu kuna kundi kubwa
la wafanyabiashara na wateja. Pia wekeni zahanati ili hawa wakipata
majeraha, wahudumiwe kwa haraka,” alisema.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa
wajasiriamali wawili, Bw. Haji Selemani na Bw. Sudi ambao walisema
wajasiriamali wote walipewa agizo la kuhamia eneo la viwanda lakini kuna
wenzao wamegoma, na wanaendelea kufanya biashara mjini ambako kuna
wateja wengi.
Akizungumza
na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa
Taifa wa Kahama, Waziri Mkuu alirudia kutoa agizo hilo na kuwaahidi
kwamba watapatiwa mafunzo ya uwezeshaji na taasisi iliyoko kwenye ofisi
yake ifikapo Julai 30, mwaka huu.
“Ifikapo
Julai 30, atakuja Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC) hapa Kahama na kutoa mafunzo ya namna ya kupata
mikopo na kufanya biashara. Haya mafunzo yatatolewa kulekule, kwa hiyo
wahini kuhamia mpate kushiriki fursa hiyo,” alisema.
Wakati
huohuo, Mkurugenzi wa Mji wa Kahama, Bw. Anderson Msumba alisema eneo
hilo la viwanda lina ukubwa wa ekari 500 na lilipimwa na kugawanywa
kisha vikapatikana viwanja 678 vyenye ukubwa wa kati, wa chini na wa juu
(high, medium and low density).
“Viwanja
hivyo wamepewa bure isipokuwa wanapaswa kulipia gharama za kupata hati
ambazo zinaanzia sh. 150,000 hadi 300,000 kutegemeana na ukubwa wa
kiwanja. Maji yapo ila yataongezwa mradi wa Zongomelo ukikamilika.”
Kuhusu
barabara za eneo hilo, Bw. Msumba alisema TARURA walishatoa makadirio
yao ambayo ni sh. bilioni 1.3 na wameshapeleka maombi hayo TAMISEMI.
Alisema maeneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo cha polisi pamoja na
mabenki, yameshatengwa, ni suala la wahusika kwenda kuomba.
No comments