Full-Width Version (true/false)


Zijue Haki za wafungwa, mahabusu wawapo gerezani

Jeshi la Magereza linasema majukumu ya msingi ya jeshi ni kuwapokea na kuwahifadhi gerezani watu wote wanaopelekwa gerezani kwa mujibu wa sheria za nchi na kuendesha programu zenye kulenga kuwarekebisha wafungwa waliohukumiwa ili watoke wakiwa raia wema.

Huduma zinazotolewa na jeshi hilo ni kwa ajili ya wafungwa wa aina zote wanaoingia magerezani, ndugu/jamaa za wafungwa, mawakili/wanasheria wa wafungwa, watu wanaotoa huduma mbalimbali kwa wafungwa zikiwamo taasisi zisizo za kiserikali na madhehebu ya dini.


Mfungwa ama mahabusu anapopokelewa gerezani kwa mara ya kwanza anayo haki ya kusomewa taratibu na sheria za magereza zitakazomuongoza awapo gerezani.


Anayo haki ya kuyaeleza matatizo yake kwa uongozi wa gereza, haki ya kupatiwa chakula kulingana na matakwa ya madhehebu yake, haki ya kutembelewa na wakili wake wakati wowote na muda wowote.


Pia haki ya kutembelewa na ndugu ama jamaa zake wakati wowote awapo mgonjwa, ana haki ya kutembelewa na polisi, lakini mfungwa akubali kuonana naye na kwa madhumuni maalumu.


Mfungwa ama mahabusu ambaye ni raia wa nchi nyingine anapopokelewa gerezani anayo haki ya kupelekewa taarifa za kuwapo kwake gerezani kwa mwakilishi/balozi wa nchi yake aliyepo nchini.


Kwa mujibu wa sheria zetu, Wafungwa wanayo haki ya kutembelewa na watu wasiozidi wawili mara moja kwa mwezi kwa muda wa dakika 15 au zaidi kwa kibali cha Mkuu wa Gereza na kwa nyakati tofauti.


Inaruhusiwa anapoingia gerezani kwa mara ya kwanza, kabla ya kuhamishiwa gereza jingine, wakati ni mgonjwa mahututi, wakati wowote kwa kibali cha Mkuu wa Gereza kama vile atakavyoona inafaa.


Wafungwa ama mahabusu wanayo haki
ya kutembelewa na wakuu wa dini kwa ajili ya ibada kulingana na madhehebu yao na haki ya kuandika au kupokea barua mara mbili kwa mwezi.


Barua zote zinazotoka na kuingia gerezani ni lazima zisanifiwe au kupitishwa na Mkuu wa Gereza.


Wafungwa ama mahabusu wanayo haki ya kutia sahihi nyaraka kwa mfano hundi, wosia na nyinginezo, haki ya kujiendeleza na masomo ya juu kulingana na sifa zake za awali kitaaluma.


Aidha, Wanayo haki ya kupata huduma ya malazi na chakula kwa viwango vilivyowekwa na Serikali na haki ya kupata huduma ya tiba na afya kwa ujumla.

No comments

Powered by Blogger.